Mmoja Afariki Dunia, mwingine ajeruhiwa kwa kupigwa risasi Kwa tuhuma za mauaji
Mmoja Afariki Dunia mwingine ajeruhiwa kwa kupigwa risasi kwa Tuhuma za Mauaji
Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya kujaribu kukwepa kukamatwa na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na makosa mbalimbali ya jinai, yakiwamo mauaji, ubakaji na unyang’anyi wa kutumia silaha. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, mtu aliyefariki dunia ametajwa kuwa Nanei Kokan (30), mkazi wa Kiji cha Parakuyo, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Kamanda Kantimbo amesema tukio hilo lilitokea Septemba 28, 2026, majira ya saa tisa alasiri, baada ya polisi kufika kijjini hapo kwa lengo la kumkamata Kokan, ambaye alikataa kukamatwa na kumshika mwanamke mmoja kama kinga huku akiwa na sime mkononi.
“Wakati akiwa amemshika yule mwanamke kama kinga ili asikamatwe, mtuhumiwa ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa akiwaambia polisi kwamba wakimsogelea atamuua mwanamke huyo. Katika harakati hizo, alipigwa risasi kwenye mkono aliokuwa ameshika sime,” amesema Kamanda Kantimbo.
Aidha, amesema katika tukio hilo, Jacob Simtoi (28), mkazi wa Parakuyo, ambaye pia anatuhumiwa kujihusisha na matukio ya mauaji, ubakaji na unyang’anyi wa kutumia silaha, alijeruhiwa kwa kupigwa risasi kwenye paja la mguu wa kulia.
Kamanda Kantimbo amesema Simtoi alijeruhiwa baada ya kujaribu kuwashambulia polisi kwa sime katika jitihada za kuwazuia wasimkamate. Amesema majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa na anaendelea kupativwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa polisi.





