Wakazi wa magomeni Kota Waishi kwa Hofu Baada ya Mfululizo wa wizi
Wakazi wa magomeni Kota Waishi kwa Hofu Baada ya Mfululizo wa wizi
Wakazi wa Magomeni Kota, Dar es Salaam, wameingiwa na hofu kufuatia mfululizo wa matukio ya wizi yanayodaiwa kutokea mchana na usiku katika majengo mbalimbali ya eneo hilo. Katika matukio hayo, wezi wanadaiwa kuvunja milango na mageti mchana, huku wengine wakiingia ndani ya nyumba usiku kupitia madirishani na kuondoka na vitu vya thamani ikiwamo televisheni, kompyuta mpakato, simu, spika, redio na fedha taslimu.
Matukio hayo tayari yameripotiwa katika Kituo cha Polisi Magomeni, huku polisi wakisema wanafuatilia ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika. Leo Alhamisi Oktoba mosi, 2026 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mtatiro Kintikwi amesema jeshi hilo linafuatilia matukio hayo na limeanza kuchukua hatua za kuimarisha usalama katika eneo hilo.
“Nitamtafuta mheshimiwa Dc (Mkuu wa Wilaya-Mtambule), kuhusu ziara hiyo ili tupange,” amesema Kintikwi, akizungumzia mpango wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule kutembelea Magomeni Kota kwa ajili ya kuzungumza na wananchi kuhusu hali ya usalama.





