Kiir Apiga Marufuku safari za Viongozi, uchaguzi wazua wasiwasi
Kiir Apiga Marufuku safari za Viongozi uchaguzi wazua wasiwasi
Wakati Sudan Kusini ikijjandaa kufanya uchaguzi mkuu uliopangwa Desemba 22, 2026, Rais Salva Kiir ameweka zuio la safari za nje kwa miezi mitatu kwa viongozi wa Serikali, maofisa wa kijeshi na vyombo vya usalama, isipokuwa wale watakaopata kibali chake.
Hatua hiyo imeongeza maswali kuhusu mazingira ya kisiasa nchini humo, ambayo yameendelea kubadilika katika kipindi cha maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kuwa wa kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 2011. Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishvwa na vyombo vya habari nchini humo, agizo hilo lilitolewa Oktoba 3, 2026, likiwataka viongozi wanaohusika kupata ruhusa ya Rais kabla ya kusafiri nje ya nchi.
Zuio hilo linawahusu maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF), kuanzia cheo cha luteni wa pili hadi jenerali, wanachama wa vyombo vingine vya ulinzi na usalama, mawaziri, makatibu wakuu wasaidizi na washauri wa Serikali.
Ingawa agizo hilo linaweka utaratibu wa kupata idhini ya Rais, muda na wigo wake vimeibua mjadala kutokana na umuhimu wa kipindi ambacho nchi hiyo inajiandaa kufanya uchaguzi. Hatua hiyo pia inakuja wakati Kiir akitafuta ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kusaidia maandalizi ya uchaguzi huo.





