Trump Kufanya Maamuzi Dhidi ya Waasi wa Houthi
Trump Kufanya Maamuzi Dhidi ya Waasi wa Houthi
Rais wa Marekani, Donald Trump amesema anafikiria uwezekano wa nchi yake kujiunga na Saudi Arabia katika mashambulizi dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen, baada ya shambulizi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa King Khalid, mjini Riyadh, kuua watu wasiopungua 12 na kujeruhi wengine 309.
Taarifa ya BBC News inaeleza Trump amesema Marekani itafanya uamuzi huo haraka, akieleza kuwa utawala wake ulikuwa umepata taarifa kuhusu shambulizi hilo muda mfupi kabla ya kutoa kauli hiyo. Miongoni mwa waliouawa ni raia mmoja wa Marekani. Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Saudi Arabia imesema waliouawa pia ni pamoja na raia wanne wa Saudi Arabia, Wabangladeshi wawili na raia mmoja mmoja wa nchi za Misri, Jordan, Syria, Palestina na Sudan.
Baadhi ya waliojeruhivwa wako katika hali mbaya. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imelaani shambulizi hilo, ikiwatuhumu waasi wa Houthi kuishambulia Saudi Arabia. Hata hivyo, waasi hao hawajathibitisha kuhusika na shambulizi la Jumamosi, licha ya kudai kuhusika na mashambulizi mengine ya awali.
Shambulizi hilo limefanyika wakati mapigano kati ya waasi wa Houthi na vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia nchini Yemen yakizidi kushika kasi. Mamlaka za Saudi Arabia zimesimamisha shughuli za uwanja huo wa ndege, huku mamia ya safari za ndege zikifutwa na kuelekezwa kwenye viwanja vingine.





