Traore Afuta Mashindano ya U-Miss Aanzisha Mashindano ya Sayansi kwa Wanawake
Traore Afuta Mashindano ya U-Miss Aanzisha Mashindano ya Sayansi kwa Wanawake
Serikali ya Burkina Faso chini ya Rais Ibrahim Traoré imechukua hatua ya kuhamasisha wasichana kujiunga na taaluma za sayansi kwa kusitisha mashindano ya urembo na kuanzisha shindano la kitaifa linalolenga kukuza vipaji vya kisayansi miongoni mwa wanawake vijana. Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na mtandao wa Afrika World, mashindano ya urembo yalisitishwa Juni 2026 wakati mamlaka zikiandaa kanuni mpya, hatua iliyolenga kulinda utamaduni wa nchi hiyo, maadili ya kijamii na heshima ya utu wa binadamu.
Aidha mnamo Agosti 2026, nchi hiyo ilizindua shindano la HAKILI Mousso, lililowakutanisha wasichana 84 kutoka maeneo mbalimbali nchini humo kushindana katika masomo ya Hisabati, Fizikia na Kemia. Washindi wa shindano hilo walipatiwa zawadi pamoja na ufadhili wa masomo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutambua na kuendeleza vipaji vya wasichana katika sayansi.
Baada ya shindano hilo, Rais lbrahim Traoré alikutana na washindi na kuwataka kujiamini, kuendeleza uwezo wao wa kisayansi na kuweka malengo makubwa katika maisha yao. Hatua hiyo imeibua mjadala kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya sayansi kwa wasichana na namna mashindano ya aina hiyo yanavyoweza kuwahamasisha vijana wengi zaidi barani Afrika kufuata taaluma za sayansi na teknolojia.





