Leo Imetimia Mwaka Mmoja Tangu Polepole Atoweke

Leo Imetimia Mwaka Mmoja Tangu Polepole Atoweke

LEO 6 Oktoba 2026, ni mwaka mmoja tangu alipotoweka aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, huku hadi sasa taarifa za uhakika kuhusu alipo zikiwa hazijawekwa wazi hadharani. Polepole, ambaye pia aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM na Mbunge wa kuteuliwa, aliripotiwa kutoweka 6 Oktoba 2025 katika eneo la Ununio jijini Dar es Salaam.

Familia yake ilisema ilikuta mlango wa nyumba aliyokuwa akiishi ukiwa umevunjwa, nyaya za umeme zikiwa zimekatwa na kulikuwa na damu ndani ya nyumba. Siku hiyo, Jeshi la Polisi lilithibitisha kuwa linafuatilia taarifa za madai ya kutekwa kwa Polepole, likisema uchunguzi ulikuwa unaendelea kubaini ukweli wa tukio hilo. Polisi pia ilisema Polepole alikuwa ametakiwa kufika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusu madai aliyokuwa ameyatoa kupitia mitandao ya kijamii.

Baadaye, mawakili wake waliwasilisha maombi ya Habeas Corpus Mahakama Kuu wakitaka suala la alipo na uhalali wa kuzuiliwa kwake lichunguzwe; maombi hayo yalikataliwa 24 Oktoba 2025, na hatua nyingine za kisheria zikafuata katika Mahakama ya Rufani. Taasisi za haki za binadamu, ikiwamo Amnesty International, zimeitaka Serikali kuweka wazi hatima na mahali alipo Polepole, huku zikieleza wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutoweshwa kwa nguvu. Mwaka mmoja baadaye, tukio hilo bado linaacha swali kubwa kwa familia, marafiki na Watanzania: Humphrey Polepole yuko wapi?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button